7 Aprili 2025 - 23:11
Source: Parstoday
Waingereza 10 wakabiliwa na tuhuma za jinai za kivita Gaza

Kundi mashuhuri la mawakili wa haki za binadamu wa Uingereza linatazamiwa kuwasilisha malalamiko ya jinai za kivita dhidi ya Waingereza kumi waliokuwa sehemu ya wanajeshi wa Israel waliofanya mashambulizi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Michael Mansfield KC, mwanachama wa kundi hilo kubwa la wanasheria wa haki za binadamu wa Uingereza, leo Jumatatu amewasilisha ripoti ya kurasa 240 kwa kitengo cha uhalifu wa kivita cha Jeshi la Polisi la Jiji la London, akiwatuhumu Waingereza hao kumi kwa kuua wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu raia wa Palestina na raia wengine wasio na hatia, sambamba na kushambulia kiholela maeneo ya raia, pamoja na hospitali.

Hati hiyo ya ufichuzi, ambayo imetayarishwa mjini The Hague, pia inawatuhumu washukiwa hao kwa khusika na mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya makaburi ya kihistoria na kuhamisha raia kwa lazima.

Mansfield, ambaye ni mashuhuri katika kesi kadhaa muhimu za kisheria amesema: "Ikiwa mmoja wa raia wetu anatenda kosa, tunapaswa kuchukua hatua dhidi ya jambo hilo.

Hata kama hatuwezi kuzuia serikali za nchi za kigeni kuwa na mienendo mibaya, lakini tunaweza angalau kuwazuia raia wetu kuwa na tabia mbaya." Mtaalamu huyo wa sheria anasema, "Raia wa Uingereza wana wajibu wa kisheria wa kutokuwa mshirika wa uhalifu unaofanyika Palestina. Hakuna aliye juu ya sheria." 

Waingereza 10 wakabiliwa na tuhuma za jinai za kivita Gaza

Timu hiyo ya wanasheria imetayarisha ripoti yake kwa niaba ya Kituo cha Sheria cha Maslahi ya Umma chenye makao yake nchini Uingereza (PILC), na Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Palestina chenye makao yake Gaza (PCHR); na imechunguza makosa yanayodaiwa kufanywa na Waingereza hao huko Gaza baina ya Oktoba mwaka 2023 hadi Mei 2024.

Ripoti hiyo ya ufichuzi inasema kuwa, Uingereza ina wajibu chini ya mikataba ya kimataifa kuchunguza na kuwashtaki wale ambao wamefanya "uhalifu wa kimsingi wa kimataifa."

Idadi kubwa ya wataalamu wa haki za binadamu na sheria wamesaini barua ya kuunga mkono hati hiyo ya ufichuzi, na wameitaka timu ya kitengo cha uhalifu wa kivita kuchunguza malalamiko hayo na kuwaadhibu wahusika kwa kuzingatia sheria.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha